Smiley face

Jumatano, 10 Januari 2018

Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee X Mungu ni Chanzo cha Uhai kwa Vitu Vyote (IV)(Sehemu ya Kwanza)


Mungu ni Chanzo cha Uhai kwa Vitu Vyote (IV)


Mwenyezi Mungu alisema, Leo, tunafanya ushirika juu ya mada maalum. Kwa kila mmoja wenu, kuna vitu viwili vikuu tu ambavyo mnapaswa kujua, kuvipitia na kuvielewa—na vitu hivi viwili ni vipi? Cha kwanza ni kuingia binafsi kwa watu katika maisha, na cha pili kinahusu kumjua Mungu. Leo Nawapa uchaguzi: Chagua kimoja. Mngependa kusikia kuhusu mada inayouhusu uzoefu wa maisha ya kibinafsi ya watu, au mngependa kusikia inayohusu kumjua Mungu Mwenyewe? Na kwa nini Ninawapa uchaguzi huu? Kwa sababu leo Ninafikiria kufanya ushirika nanyi juu ya mambo mapya kuhusu kumjua Mungu. Lakini, hata hivyo, kwanza nitawaacha mchague kimoja kati ya vitu viwili ambavyo Nimezungumzia hivi punde. (Ninachagua kuhusu kumjua Mungu.) (Tunafikiri kwamba kufanyia ushirika maarifa ya Mungu ni bora pia.) Mnadhani mambo ambayo tumekuwa tukiyafanyia ushirika hivi karibuni kuhusu kumjua Mungu yanawezekana? (Mungu alipokuwa na ushirika wa kwanza, hatukuhisi itawezekana. Baada ya hapo Mungu alifanya ushirika mara kadhaa, na tuliporejelea ushirika wa kwanza, katika mazingira yaliyoumbwa na Mungu, ndugu na dada wakawa makini kwa uzoefu katika eneo hili.) Ni haki kusema kuwa ni nje ya uwezo wa watu wengi. Mwaweza kukosa kusadiki maneno haya. Kwa nini Ninasema hili? Kwa sababu mlipokuwa mkisikiliza Niliyokuwa nikisema awali, haijalishi Niliyasema vipi, au ni kwa maneno gani, mlipoyasikia, moja kwa moja na kinadharia mlikuwa mnatambua Nilichokuwa nikisema, lakini tatizo lenu kubwa ni kwamba, hamkuelewa ni kwa nini Niliyasema mambo haya, ni kwa nini nilizizungumzia hizi mada. Hiki ndicho kiini cha hili suala. Na kwa hiyo, japo kusikia kwenu haya mambo kuliongeza na kuimarisha uelewa wenu kuhusu Mungu na matendo Yake, kwa nini bado mnapata ugumu kumjua Mungu? Sababu ni hii: baada ya kusikia Nilichokisema, wengi wenu hawaelewi ni kwa nini Nilisema hili, na lina uhusiano gani na kumjua Mungu. Au sivyo? Ugumu wenu wa kuelewa uhusiano wake na kumjua Mungu unahusu nini? Mmewahi kuliwazia hili? Huenda hamjawahi. Sababu ya kutoelewa mambo haya ni kwa sababu uzoefu wenu wa kimaisha ni wa juujuu sana. Ikiwa ufahamu na uzoefu wa watu kuhusu maneno ya Mungu utabaki kuwa wa juujuu, basi ufahamu wao mkubwa kuhusu Mungu utakuwa si yakini na kidhahania—utakuwa wa hali ya chini, wa kimafundisho, na wa kinadharia. Kinadharia, yanaonekana au kusikika kuwa na mantiki na razini, ila ufahamu kuhusu Mungu utokao vinywani mwa watu ni mtupu. Na mbona Ninasema kuwa ni mtupu? Kwa sababu, kwa hakika, moyoni mwako hauko wazi kama maneno kuhusu kumjua Mungu yatokayo kinywani mwako ni sawa au la, ikiwa ni sahihi au la. Hivyo basi, japo watu wengi wamesikia taarifa na mada nyingi kuhusu kumjua Mungu, ufahamu wao kuhusu Mungu haujatoka nje ya nadharia na mafundisho ya yasiyo yakini na dhahania.
Kwa hiyo hili tatizo linaweza kusuluhishwa vipi? Je, mmewahi kuliwazia hilo? Ikiwa watu hawautafuti ukweli, wanaweza kuwa na uhalisi? (Hawawezi.) Sawa. Kwa hakika hawawezi. Ikiwa watu hawautafuti ukweli, basi bila shaka hawana uhalisi, na hivyo, kwa hakika hawana ufahamu au uzoefu wa maneno ya Mungu. Je, yawezekana wasioyafahamu maneno ya Mungu wamfahamu Mungu? Hawawezi Kabisa! Haya mawili yameshikamana. Hivyo, watu wengi husema, “Kumjua Mungu kwawezaje kuwa kugumu hivi? Mbona ni kugumu sana? Mbona nisiseme chochote kuhusu kumjua Mungu?” Mnapozungumzia kujijua nyinyi wenyewe, mnaweza kuzungumza kwa saa nyingi, ila mnapozungumzia kumjua Mungu mnakoswa maneno. Hata mnapoweza kusema machache, ni kwa kushurutishwa, yanakosa uchangamfu—hata yanasikika ya kufedhehesha mnapojisikia mkiyasema. Hiki ndicho chanzo. Ukihisi kwamba kumjua Mungu ni kugumu sana, kwamba kunakuchosha, kwamba huna la kuzungumzia—huna chochote cha kufanya ushirika na kuwapa wengine, na kujipa wewe mwenyewe—basi hili linathibitisha kwamba hujayapitia maneno ya Mungu. Maneno ya Mungu ni nini? Je, maneno ya Mungu sio maonyesho ya kile Mungu anacho na alicho? Ikiwa hujapitia uzoefu wa maneno ya Mungu, unaweza kuwa na ufahamu wowote kuhusu anacho na alicho. Kwa hakika siyo, sawa? Vitu hivi vyote vimeshikamana. Ikiwa huna uzoefu wa maneno ya Mungu, basi huwezi kuelewa mapenzi ya Mungu, na hutajua tabia Yake ni nini, Anachokipenda, Anachokichukia, mahitaji Yake kwa mwanadamu ni yapi, mtazamo Wake kwa walio wazuri, na kwa wale walio waovu ni upi—kwa hakika haya yote yatakuwa tata na yenye mashaka kwako. Ikiwa mnamwamini Mungu katikati ya haya mashaka, wakati mnaposema kuwa nyinyi ni miongoni mwa wale wanaoutafuta ukweli na kumfuata Mungu, je, haya maneno yana uhalisi? Hayana! Hivyo, sasa, fanyani uamuzi wenu: Mnachagua mada gani leo? (Kuingia katika maisha na uzoefu wa maisha wa mtu binafsi.) (Tunachagua kuingia katika maisha.) Ni vipengele vipi vya mada ambavyo hamvifahamu kuhusu kuingia katika maisha? Je, mioyo yenu inawaambia kitu chochote? Bado hamjui, je mwajua? Je, dada na ndugu wengine wamechagua mada gani? Mngependa kusikia kuhusu kumjua Mungu, au kuhusu uzoefu wa maisha? (Tungependa kusikia kuhusu kumjua Mungu.) (Kumjua Mungu.) Sawasawa, wengi wenu mmechagua kumjua Mungu. Hivyo tuendelee kufanya ushirika kuhusu kumjua Mungu.
Nyinyi nyote mna shauku ya kuisikia mada tutakayoifanyia ushirika, sivyo? Mada tutakayowasiliana kwa karibu leo pia inahusiana na mada ya “Mungu ni chanzo cha uhai kwa vitu vyote” ambayo tumekuwa tukizungumzia hivi karibuni. Tumekuwa na mazungumzo kadhaa kuhusu “Mungu ni chanzo cha uhai kwa vitu vyote,” ambayo makusudi yake yalikuwa kutumia njia na mitazamo mbalimbali kuwaarifu watu jinsi Mungu anatawala juu ya vitu vyote, ni kwa njia gani Anavitawala vitu vyote, na ni kwa kanuni gani anavisimamia vitu vyote, ili kwamba viweze kuishi katika hii sayari Aliyoumba Mungu. Tulizungumza pia mengi kuhusu jinsi ambavyo Mungu anamkimu mwanadamu: ni kwa njia gani Mungu anamkimu mwanadamu, ni mazingira ya kuishi ya aina gani Mungu anampa mwanadamu, na ni kwa njia na nguvu gani Anampa mwanadamu mazingira thabiti ya kuishi. Japo Sikuzungumzia moja kwa moja uhusiano baina ya utawala wa Mungu juu ya vitu vyote, uendeshaji Wake wa vitu vyote na usimamizi Wake, kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja Nilisema ni kwa nini Anaviendesha vitu vyote namna hii, na ni kwa nini Anamkimu na kumlisha mwanadamu namna hii—yote ambayo yanahusu usimamizi wa Mungu. Maudhui tuliyoyazungumzia yalikuwa mengi na mapana—kuanzia mazingira makubwa hadi vitu vidogo zaidi kama mahitaji na lishe ya msingi ya wanadamu; kuanzia jinsi Mungu anaviongoza vitu vyote na kuvifanya vitende kazi kwa utaratibu, hadi kwenye mazingira ya kuishi sahihi na ya kufaa Aliyoyaumba kwa ajili ya watu wa kila rangi, na kadhalika. Haya maudhi mapana yanahusu jinsi mwanadamu anaishi katika mwili. Hivi ni kusema, yote yanahusiana na vitu katika ulimwengu halisi vinavyoonekana kwa macho ya kawaida, na ambavyo mwanadamu anaweza kuvihisi, kwa mfano, milima, mito, bahari, tambarare… Hivi vyote ni vitu vinavyoweza kuonekana na kuguswa. Nizungumzapo kuhusu hewa na halijoto, mnaweza kutumia pumzi zenu kuhisi moja kwa moja uwepo wa hewa, na miili yenu kuhisi kama halijoto iko juu au chini. Miti, nyasi, na ndege na wanyama porini, vitu vinavyopaa angani, na kutembea ardhini, na wanyama wadogo mbalimbali watokezao kutoka matunduni, vyote vinaweza kuonekana kwa wanadamu kwa macho yao wenyewe na kusikika kwa masikio yao wenyewe. Japo mawanda ya vitu kama hivyo ni mapana, miongoni mwa vitu vyote vinawakilisha tu ulimwengu halisi. Kwa wanadamu, ni vitu gani vyaweza kuonekana? Ni vitu yakinifu. Vitu yakinifu ni vitu ambavyo watu wanaweza kuviona na kuvihisi, yaani, ukivigusa, utavihisi, na macho yako yakiviona, ubongo wako utakupatia umbo, picha. Ni vitu ambavyo ni halisi na kweli; kwako si dhahania, bali vina umbo na picha; vinaweza kuwa mraba, au duara, au virefu au vifupi, vikubwa au vidogo; na kila kimoja kinakupa taswira tofauti. Vitu hivi vyote vinawakilisha ile sehemu ya vitu ambayo ni ulimwengu yakinifu. Na hivi, “vitu vyote” katika “utawala wa Mungu juu ya vitu vyote” vinajumuisha nini kwa Mungu? Havijumuishi tu vitu ambavyo watu wanaweza kuona na kugusa, bali, vilevile, visivyoonekana na visivyoshikika. Hii ni mojawapo ya maana za kweli za utawala wa Mungu juu ya vitu vyote. Hata kama vitu hivi havionekani na havigusiki na watu, ni ukweli ambao upo. Kwa Mungu, almradi vinaweza kuonekana kwa jicho Lake na vipo ndani ya ukuu Wake, kwa hakika vipo. Hata kama, kwa mwanadamu, ni dhahania na visivyofikirika—na hata kama, aidha, havionekani na havishikiki—kwa Mungu kwa kweli na kwa kwa uhalisi vipo. Huo ndio ulimwengu mwingine wa vitu vyote ambavyo Mungu anatawala, na ni sehemu nyingine ya mawanda mengine ambayo Anatawala. Hii ndiyo mada ambayo tutaifanyia ushirika leo—jinsi Mungu anatawala na kuuongoza ulimwengu wa kiroho. Kwa kuwa mada hii inagusia jinsi Mungu anatawala na kusimamia vitu vyote, inahusiana na ulimwengu ulio nje ya ulimwengu yakinifu—ulimwengu wa kiroho—na kwa hivyo ni muhimu sana kwetu kuuelewa. Ni baada tu ya kushiriki na kuelewa ndipo watu wanaweza kuelewa kwa hakika maana ya kweli ya maneno “Mungu ni chanzo cha uhai kwa vitu vyote.” Na shabaha ya mada hii ni kukamilisha dhamira ya “Mungu anavitawala vitu vyote, na Mungu anavisimamia vitu vyote.” Pengine, mtakapoisikia mada hii, inaweza kuonekana ni ya ajabu na isiyoaminika kwenu—lakini bila kujali mnavyohisi, kwa kuwa ulimwengu wa kiroho ni sehemu moja ya vitu vinavyotawaliwa na Mungu, ni sharti mjifunze kitu kuhusu mada hii. Baada ya kujifunza, mtakuwa na ufahamu wa kina, uelewa na maarifa kuhusu maneno “Mungu ni chanzo cha uhai kwa vitu vyote.”

1. Jinsi Mungu Anatawala na Kuongoza Ulimwengu wa Kiroho

Kwa ulimwengu yakinifu, watu wakikosa kuelewa vitu au jambo fulani wanaweza kufungua kitabu na kutafuta taarifa mwafaka, vinginevyo wanaweza kutumia njia mbalimbali kubaini asili ya habari kuvihusu. Lakini inapokuja kwa ulimwengu huu mwingine ambao tunauzungumzia leo—ulimwengu wa kiroho ulio nje ya ulimwengu yakinifu—watu hawana hasa mbinu au njia za kujifunzia maana ya mambo na ukweli wake. Mbona Ninasema hivi? Kwa sababu, katika ulimwengu wa mwanadamu, kila kitu cha ulimwengu yakinifu hakijitengi na uwepo wa kimwili wa mwanadamu, na kwa sababu watu wanahisi kwamba kila kitu katika ulimwengu yakinifu hakitenganishwi na maisha yao ya kimwili na uhai wao wa kimwili, watu wengi wanafahamu tu kuhusu, au kuona, vitu yakinifu mbele ya macho yao, vitu vinavyoonekana kwao. Bali inapokuja katika ulimwengu wa kiroho—yaani, kila kilicho cha ule ulimwengu mwingine—ni haki kusema kuwa watu wengi hawaamini. Hiyo ni kwa sababu hauonekani kwao, na wanaamini kuwa hakuna haja ya kuuelewa, au kujua kitu chochote kuuhusu, kutosema chochote jinsi huu ulimwengu wa kiroho ni ulimwengu tofauti kabisa na ulimwengu yakinifu. Kwa Mungu, uko dhahiri, lakini kwa mwanadamu umejificha na si dhahiri, na kwa hiyo watu wanakuwa na ugumu kupata njia ambayo kupitia kwayo wanaweza kuelewa vipengele mbalimbali vya ulimwengu huu. Mambo Nitakayoyasema kuhusu ulimwengu wa kiroho yanahusu utawala na ukuu wa Mungu tu. Bila shaka yanahusiana pia na matokeo na hatima ya mwanadamu—lakini Sifichui miujiza, wala Siwambii siri zozote mnazotaka kugundua, kwani hili linahusu ukuu wa Mungu, utawala wa Mungu, na riziki ya Mungu, na kwa hivyo Sitazungumzia tu sehemu ambayo ni muhimu nyinyi kuijua.
Kwanza, hebu Niwaulize swali: katika mawazo yenu, ulimwengu wa kiroho ni nini? Kuzungumza kwa ujumla, ni ulimwengu ulio nje ya ulimwengu yakinifu, ambao hauonekani na haushikiki na watu. Lakini kwa fikra zenu, ulimwengu wa kiroho unafaa uwe ulimwengu wa aina gani? Pengine, kwa sababu ya kutoweza kuuona, mnaweza kushindwa kuufikiria. Lakini mtakaposikia hadithi kuuhusu, bado mtafikiri, hamtaweza kujizuia nyinyi wenyewe. Na kwa nini Ninasema hili? Kuna kitu kinachowatokea watu wengi wanapokuwa wachanga: mtu akiwasimulia hadithi ya kuogofya—juu ya mazimwi, na roho—wanaogopeshwa kabisa. Na kwa nini wanaogopeshwa? Ni kwa kuwa wanavifikiria vitu hivyo; hata japo hawawezi kuviona, wanahisi kuwa vipo kila pembe ya chumba chao, vimejificha sehemu fulani, au sehemu fulani yenye giza, na wanaogopa sana kiasi kwamba hawawezi kuthubutu kulala. Hasa wakati wa usiku, hawathubutu kuwa chumbani peke yao, au uani peke yao. Huo ndio ulimwengu wa kiroho wa fikra zenu, na ni ulimwengu ambao watu hudhani unaogofya. Kila mtu ana fikra fulani, na kila mtu anaweza kuhisi kitu.
Hebu tuanze na ulimwengu wa kiroho. Ulimwengu wa kiroho ni nini? Hebu Niwape maelezo mafupi na rahisi. Ulimwengu wa kiroho ni sehemu muhimu, ambayo ni tofauti na ulimwengu yakinifu. Na mbona Ninasema kwamba ni muhimu? Tutalizungumzia hili kwa kina. Uwepo wa huu ulimwengu wa kiroho umeungana na ulimwengu yakinifu wa mwanadamu kwa njia isiyoweza kufumbulika. Una jukumu katika mzunguko wa uhai na mauti wa mwanadamu katika utawala wa Mungu juu ya vitu vyote; hili ndilo jukumu lake, na sababu mojawapo inayofanya uwepo wake kuwa muhimu. Kwa sababu ni mahali ambapo hapawezi kutambuliwa kwa milango mitano ya fahamu ya mwanadamu, hakuna anayeweza kubaini kwa hakika kuwepo au kutokuwepo kwake. Shughuli za ulimwengu wa kiroho zimeunganika kikamilifu na uwepo wa mwanadamu, na kwa sababu hiyo jinsi mwanadamu anaishi inaongozwa kwa kiwango kikubwa na ulimwengu wa kiroho. Je, hili linahusiana na ukuu wa Mungu? Linahusiana. Nisemapo hili, unaelewa ni kwa nini Ninajadili mada hii; Kwa sababu inahusu ukuu wa Mungu, na utawala Wake. Katika ulimwengu kama huu—ulimwengu ambao hauonekani kwa watu—kila sheria yake ya peponi, amri na mfumo wake wa utawala ni wa juu zaidi kuliko sheria na mifumo ya nchi yoyote katika ulimwengu yakinifu, na hakuna kiumbe aishiye katika ulimwengu huu anaweza kuzivunja au kujitwalia bila haki. Je, hili linahusiana na ukuu na utawala wa Mungu? Katika ulimwengu huu kuna amri wazi za utawala, sheria wazi za mbinguni, na masharti wazi. Katika viwango tofauti na katika mawanda tofauti, wasimamizi huzingatia kikamilifu katika wajibu wao na kufuata sheria na masharti, kwa kuwa wanajua matokeo ya kukiuka sheria ya mbinguni ni yapi, wanafahamu wazi jinsi ambavyo Mungu anaadhibu maovu na kutuza mazuri, na kuhusu jinsi Anavyoviendesha vitu vyote, jinsi Anavyotawala vitu vyote, na zaidi, wanaona wazi ni jinsi gani Mungu anaendesha sheria za mbinguni na masharti Yake. Je, hizi ni tofauti na ulimwengu yakinifu unaokaliwa na wanadamu? Ni tofauti kwa kiasi kikubwa. Ni ulimwengu ambao ni tofauti kabisa na ulimwengu yakinifu. Kwa kuwa kuna sheria na masharti ya mbinguni, inahusu ukuu wa Mungu, utawala, aidha, tabia ya Mungu ya kile Anacho na alicho. Baada ya kusikia hili, hamhisi kwamba ni muhimu sana Mimi kuzungumzia hii mada? Hamtamani kujifunza siri zilizomo? Hiyo ndiyo dhana ya ulimwengu wa kiroho. Japo unapatikana sambamba na ulimwengu yakinifu, na wakati ule ule ukiwa chini ya utawala na ukuu wa Mungu, utawala na ukuu wa Mungu ya huu ulimwengu ni makali zaidi kuliko ulivyo ulimwengu yakinifu. Ikija katika maelezo, tunafaa tuanze na jinsi ulimwengu wa kiroho unawajibikia kazi ya mzunguko wa uhai na mauti ya mwanadamu, kwa kuwa kazi hii ni sehemu kuu ya viumbe wa ulimwengu wa kiroho.
Miongoni mwa wanadamu, Ninawaainisha watu katika aina tatu. Aina ya kwanza ni wasioamini, wale wasio na imani za kidini. Wanaitwa wasioamini. Wengi wa wasioamini wanaamini tu katika pesa, wanatafuta tu maslahi yao wenyewe, wana tamaa ya vitu, na wanaamini katika ulimwengu yakinifu, si katika mzunguko wa uhai na mauti au katika semi za miungu na mapepo. Ninawaainisha kama wasioamini na ni wa aina ya kwanza. Aina ya pili ni watu mbalimbali wenye imani tofauti na wasioamini. Miongoni mwa wanadamu, Ninawagawa hawa wenye imani katika aina kuu kadhaa: Ya kwanza ni Wayahudi, wa pili ni Wakatoliki, ya tatu ni Wakristo, ya nne ni Waislamu, na ya tano ni wafuasi wa Budha—kuna aina tano. Hizi ndizo aina mbalimbali za watu wenye imani. Aina ya tatu ni wale wanaomwamini Mungu, inayohusiana nanyi. Hii sampuli ya waumini ni wale wanaomfuata Mungu leo. Hawa watu wamegawanyika katika aina mbili. Wateule wa Mungu na watendaji-huduma. Sawa! Hizi aina kuu zimebainishwa wazi. Basi sasa, akilini mwenu mnaweza kutofautisha wazi aina na madaraja ya binadamu. Wa kwanza ni wasioamini—nimesema wasioamini ni watu gani. Wengi wa wasioamini wanamwamini yule Mzee aliye Angani; wanaamini kuwa upepo, mvua na radi vyote vinadhibitiwa na huyu Mzee aliye Angani, ambaye wanategemea kwa upanzi wa mimea na uvunaji wa mazao—bali kwa kutaja imani kwa Mungu wanapoteza hamu. Je, hii yaweza kuitwa imani kwa Mungu? Watu kama hao wanahesabiwa katika wasioamini. Wale ambao hawamwamini Mungu na kumwamini tu Mzee aliye Angani wote ni wasioamini; wale wote wasioamini, au kumfuata Mungu, ni wasioamini. Aina ya pili ni wale wote walio katika dini tano kuu duniani na wanaomwamini Mungu asiye yakini. Aina ya tatu ni wale wanaomwamini Mungu wa vitendo ambaye Amekuwa mwili katika siku za mwisho—ambao wanamfuata Mungu leo. Na kwa nini Nimewagawa wanadamu wote katika aina hizi? (Kwa sababu wana vituo na hatima tofautitofauti.) Hicho ni kipengele kimoja. Kwa sababu, wakati haya matabaka na aina mbalimbali za watu wanarudi katika ulimwengu wa kiroho, kila mmoja atakuwa na sehemu tofauti ya kuenda, watapitia sheria ya mzunguko tofauti wa uhai na mauti na hii ndiyo sababu Nimewaainisha wanadamu katika hizi aina kuu.
Februari 15, 2014
kutoka kwa Mwendelezo wa Neno Laonekana katika Mwili
Kujua zaidi:  Kuhusu Kanisa la Mwenyezi Mungu,  Umeme wa Mashariki

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni